Teknolojia ya uvunaji wa maji: Kumaliza tatizo la uhaba wa chakula nchini

Daktari Esther Gikonyo/Picha:Robert Malala

By RUTH KEAH

Shirika la kilimo na utafiti la Kenya (KALRO) tawi la Kabete linapatikana takriban kilomita 13 kutoka jijini Nairobi nchini Kenya.

Upande wa kulia mita chache tu baada ya kuingia kwenye lango kuu,unakutana na shamba lenye ukubwa wa ekari moja. Lilikuwa kivutio kikuu kwa watu waliotembelea shirika hilo siku ya maonyesho ya kilimo.

Hii ni kutokana na mazao yaliyonawiri, sio tu kwa rangi yake ya kupendeza ya kibichi, bali pia kwa ubora wa mazao hayo licha ya kuwa ni msimu wa kiangazi.

Shirika hilo,limekuwa likitumia teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua, na kisha kunyunyuzia shamba hilo.

Daktari Esther Gikonyo ni mkurugenzi mkuu wa shirika la KALRO tawi la Kabete,yeye pia ni mtaalamu katika sekta ya rotuba ya udongo.

Alisema teknolojia hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa wakulima wanatumia ili kuvuna chakula cha kutosha.

Daktari Esther Gikonyo alisema,kama shirika, walilima shamba hilo mwezi wa Januari na Februari na kunyunyizia maji mazao hayo kwa kutumia maji ambayo walivuna.

Alisema endapo jamii itakumbatia teknolojia ya uvunaji wa maji, basi kila familia itaweza kujitegemea kwa kupata chakula kila siku.

Zaidi, Daktari Gikonyo aliwashauri wakulima kujenga tabia ya kuvuna maji ya mvua hasa katika kipindi ambacho mvua ni chache na haziendani na kalenda ya wakulima.

Sawia kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa yakisababisha kukosekana kwa mvua za kutosha na uharibifu wa mazingira.

Hali hiyo imewasababisha wakulima kupata mazao kidogo ama kutovuna kabisa.

Jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi ya maeneo nchini kuwa hatarini kukumbwa na baa la njaa.

 Uvunaji wa maji ya mvua.

Uvunaji wa maji ni mbinu ambayo inazuia maji ya mvua kutiririka hovyo.

Badala yake, maji hukusanywa na kuhifadhiwa na kutumiwa baadaye na watu,wanyama ama kwa kunyunyizia mimea

Francis Karanja ni mhandisi, pia ni mtaalamu anayehusika na teknolojia ya uvunaji wa maji.

Mhandisi Karanja alisema teknolojia hiyo ya uvunaji wa maji ni rahisi na kila mkulima anaweza kuimudu.

“Baadhi ya vifaa ambavyo tulitumia ni karatasi nyeusi ya kufunika bwawa, matangi mawili ya maji ambayo huvutwa kwa kutumia nguvu za miale ya jua.”

Kulingana na mhandisi Karanja, bwawa hilo lina uwezo wa kubeba maji lita 4,500.

Na linaweza kulima shamba la ukubwa wa ekari moja kwa kipindi cha miezi mitatu kukuza aina tofauti tofauti ya mboga.

Mhandisi Karanja alisema bwawa hilo liliwagharimu takriban shilingi laki mbili na elfu hamsini. Huku likitarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka kumi.

Washikadau mbalimbali walionyesha teknolojia mbalimbali wanazotumia kufanya ukulima.

Baadhi yao ni wanafunzi kutoka shule ya msingi ya Kangemi jijini Nairobi.

Wanafunzi walio kwenye kikundi cha kilimo cha 4K Club, wakionyesha weledi wao wa kukuza mazao hasa mboga kupitia teknolojia mbalimbali.

Huku wakitumia maji hayo yaliyovunwa kukuza mboga zao.

Makala haya yamefanikishwa kwa usaidizi kutoka kwa muungano wa wanahabari wanaoandika habari za sayansi(MESHA).

 
 
 
 
 
 
 

Subscribe to Post Updates

Tags: No tags

Leave A Comment